Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kitabu cha Cycles of American kilichotungwa na Arthum
Schelesinger Jr kinasema kutokufungwa na mawazo ya kale katika mazingira
yanayobadilika kunampa kiongozi wa kidemokrasia nafasi ya kutengeneza
vionjo vitamu ili apendwe na kufurahiwa na wengi.
Wanasiasa wetu wengi wao ni watu wenye woga wa
mabadiliko, wanavyochukia mabadiliko ya kifikra ni kama vile mtoto
achukiavyo kuchomwa sindano na daktari. Hawapendi fikra mbadala na wala
kubadilika.
Namchukulia kiongozi wa zamani katika Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Hassan
Nassor Moyo kuwa ni miongoni mwa viongozi wasiofungwa na mawazo ya kale
na aliyekuwa tayari kukabili changamoto za mawazo kinzani kwa hoja.
Ijapokuwa kwa wakati huu hayupo tena katika ulingo
wa kisiasa, lakini Mzee huyu anabaki kuwa mtumishi wa wananchi aliejipa
wajibu wa kuisadia jamii kuondokana na mazonge ya fikra za ukale hasa
wanapokabili jambo lenye kugusa masilahi ya nchi na wananchi kwa ujumla.
Mchakato wa katiba mpya umemkuta Mwanasiasa huyo
mkongwe mahiri, shupavu na hodari akiwa mwenye afya na siha njema ambaye
kwa sababu ya ari ya kupenda nchi yake hana kago ya kukaa pembezoni.
Hapendi awe nje ya uwanja kubaki mtazamaji katika
jambo ambalo angeweza kushiriki na kusaidia hususan jamii ya vijana
ambayo kwa namna moja au nyingine si mashuhuda wa Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar.
Alivyokuwa kila Mtanzania kuwa na ari ya kutaka
mabadiliko ya muundo wa Muungano, ndivyo alivyo Mzee Hassan Nassor Moyo.
Mara kadhaa nilipokutana na kubadilisha mawazo, alinieleza kuwa yeye si
mtu wa kufungika kimawazo.
Bila shaka anaungana na Sheikh Shaaban Robert
katika kitabu chake cha Kusadikika alipoandika “Nashikilia ukale kama ni
lazima na huuacha vilevile ikiwa haunifai. Nitaendeleza kubadili mambo
kwa sababu siwezi kuwa mtumwa wa kutenda hayo kwa hayo nikazuia bidii
yangu. Ukale huniletea mashaka nikajidai kuwa ni wajibu wangu”.
Mzee Moyo hashikilii ukale akazuia mabadiliko ya
leo na ya miaka hamsini ijayo. Amekuwa miongoni mwa wanasiasa walioweka
wazi misimamo yao kuhusu ulazima wa mabadiliko katika Muungano.
Viunga vya Zanzibar na Tanzania Bara kwa jumla
vinatokota kwa hoja ya Muungano, hakuna asiyejuwa jambo hilo, kila kona,
lakini mbona kila nikitafakari sauti hizi nahisi kama vile wasemaji
wake wanaotaka mabadiliko katika mfumo wa muundo wa Muungano hoja zao ni
zenye mantiki na zisizotakiwa kukejeliwa?
Hivi unawazaje kukataa ukweli kwamba mfumo wa
muundo wa Muungano una matatizo na tunalazimika kubadili? Kutoa hoja ya
kutaka mabadiliko imekuwa nongwa kiasi cha watu kuchukiana, kuhasimiana
au kuvunjiana heshima hadharani?
Ikiwa mtu anaamini kuwa ana nguvu ya watu
inayomuunga mkono katika hoja yake, ya nini kuweweseka? Tusubiri kura ya
maoni itakuja na kila mwenye haki atapiga kura na kuamua, hapo ndipo
itajulikana wazi kuwa wale waliokuwa wakipiga porojo na wale waliokuwa
wakitoa hoja zenye mantiki.
Baadhi ya watu hawana hesabu nzuri, pungufu kwao kamili, wana macho hayaoni, wana masikio hayasikii, wana akili hawazitumii.
Watu shupavu na wenye misimamo, mara zote hawaogopi kuadhibiwa kwa misimamo yao au mitazamo ya fikra zao.
Unawazaje kubeza mawazo ya Mzee Moyo ambaye Baraza
la Kwanza la Mawaziri katika Jamhuri ya Watu wa Zanzibar mwaka 1964
alikuwa Waziri mdogo na baadye kuwa Waziri kamili katika SMZ na SMT.
Uzoefu wake serikalini na katika Chama cha
Mapinduzi kabla ya hapo Afro Shiraz Party unatosha kuyapa uzito yale
anayoyashauri kuhusu katiba mpya kwani ni yeye akiwa na wajumbe wengine
kutoka ASP na TANU waliofanikisha kuunganishwa kwa vyama hivyo na
kuzaliwa kwa CCM.
Tukumbuke kuwa wanachama wengi wa ASP walipinga
wazo la kuunganisha vyama. Lakini kwa sababu ya dhamira ya umoja, Mzee
Moyo, marehemu Sheikh Thabit Kombo Jecha na mwenyewe Rais wa pili wa
Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi
walifanikisha lengo hilo. Kadi ya CCM ya Mzee Moyo haipindukii namba
kumi.
“Vijana wangu nataka kuwaeleza kuwa suala kubwa ni
nchi, chama lilikuwa jambo la pili na kama viongozi wetu wa chama
wanataka kutupeleka huko tukaeleze msimamo wa Chama, mimi nasema
Muungano umekuja kwanza na hivyo ndiyo ninavyojua mimi na huo ndio
msimamo wangu” Anasema Mzee Moyo.
Maelezo haya ya Mzee Moyo hayakuwa ni maneno ya
porojo au mazungumzo ya “Alfu Lela Ulela bali anatumia uwezo na uzoefu
wake kuelezea kero za Muungano, faida yake na wapi Wazanzibari waelekee
katika kupata mfumo wa muundo wa Muungano wenye usawa kupitia Katiba
Mpya
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment