Home » » SHEIN:ZANZIBAR KUWA NA MADAKTARI WA KUTOSHA

SHEIN:ZANZIBAR KUWA NA MADAKTARI WA KUTOSHA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, akizungumza na ujumbe wa viongozi wa afya kutoka Cuba unaoongozwa na Naibu Waziri wa Ufundishaji na Utafiti katika Wizara ya Afya ya Jamii Cuba, Dk. Marieta Cutino Redriguez pamoja na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Jorge Luis Lopez Tormo, walipokutana na Rais Ikulu mjini Zanzibar jana.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein amesema miaka michache ijayo Zanzibar itakuwa na madaktari wa kutosha kufikia uwiano uliopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) wa angalau daktari mmoja kuhudumia watu 10,000  kwa nchi zinazoendelea.
Dk. Shein aliyasema hao juzi katika mahafali ya kwanza ya Skuli ya  Udaktari ya Zanzibar inayoendeshwa kwa ushirikiano na chuo kikuu cha Matanzas cha Cuba yaliyofanyika Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni mjini Unguja.

Katika mahafali hayo wanafunzi wa udaktari 38 ambao walichukua mafunzo yao Zanzibar na nchini Cuba,  walikabidhiwa shahada zao za udaktari kutoka kwa Mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Matanzas Dk. Luis Ulpiano Perez Marques.

Dk. Shein aliwaeleza wahitimu na wageni waliohudhuria mahafali hayo kuwa kuhitimu madaktari hao 38 kwa mpigo  Zanzibar ni ushahidi wa kutosha kuwa SMZ, imekuwa ikitekeleza kwa vitendo azma yake ya kuwapatia wananchi wake huduma bora za afya.

Alifafanua kuwa mwanzoni mwa mwaka huu,  uwiano wa daktari Zanzibar ulikuwa watu 18,982 lakini baadhi ya kuhitimu kwa madaktari hao,  kumeleta mabadiliko katika uwiano huo.

Hata hivyo,  alisema kipindi kifupi kijacho vijana wengi waliopelekwa kusomea udaktari nchi za nje  na Tanzania Bara,  watamaliza masomo yao na kuongeza idadi ya madaktari,  hivyo kupunguza pengo la uwiano huo.

Dk. Shein alisema SMZ iliweka lengo la daktari mmoja kuhudumia watu 6,000 na kuwa hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kutekeleza lengo hilo.

Alimshukuru  Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume kwa ziara yake nchini Cuba mwaka 2006  kuzaa skuli hiyo ya udaktari.

Naye Balozi wa Cuba nchini, Jorge Luis Lopez Tormo alipongeza jitihada za pamoja kati ya wahadhiri na madaktari wa Cuba na SMZ kupitia Wizara ya Afya kwa mafanikio hayo.

Awali akitoa maelezo katika mahafali hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Saleh Mohamed Jidawi, alisema mafunzo hayo yamegharimiwa kwa kiwango kikubwa na SMZ na kueleza kuwa ina mpango wa kuwapatia madaktari hao mafunzo zaidi ili kupata mabingwa katika fani mbalimbali za afya.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa