Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameelezea kushangazwa na tabia ya vyama vya upinzani kususia mchakato wa Katiba wakati ndio waliokuwa mstari wa mbele kulilia uwepo wa Katiba mpya. Aidha, ameelezea kushangazwa na msimamo wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuikataa Katiba Inayopendekezwa, ilhali mambo anayoyalilia yamo katika katiba hiyo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara Uwanja wa Demokrasia mjini hapa alisema Katiba Inayopendekezwa imetoa fursa kubwa kwa Zanzibar kufanya mambo yao kwa mapana zaidi ikiwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema Katiba Inayopendekezwa ni kwa maslahi ya Watanzania ambayo imezingatia mambo yote muhimu ikiwemo kwa upande wa Zanzibar.
Alisema: “Nimesikitishwa sana mwenzangu, Makamu wangu wa Kwanza wa Rais amekuwa akisisitiza kutungwa kwa sera za nishati na mafuta kwa ajili ya kujitayarisha kuchimba mafuta, lakini yeye Katiba Inayopendekezwa haikubali.”
Akifafanua zaidi alisema Baraza la Wawakilishi ndiyo lililopitisha azimio la kutaka nishati ya mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano. Aidha, alimtaka Maalim Seif kuacha kuwashawishi wananchi wa Zanzibar kuikataa Katiba Inayopendekezwa akisema yeye sio msemaji wa wananchi wa Zanzibar.
“Msemaji wa wananchi wa Zanzibar wote ni mimi na sio yeye…nawataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ya kuipitisha Katiba mpya Inayopendekezwa,” alisema.
Alisema Katiba Inayopendekezwa imezingatia mambo yote ambayo wananchi wa Zanzibar wametaka kuzingatiwa na kusisitizwa ikiwemo mafuta na gesi.
Alisisitiza na kusema Katiba Inayopendekezwa imezingatia na kuuenzi Muungano wa Tanganyika wa Zanzibar pamoja na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambayo yameasisiwa na viongozi wakuu wa nchi mbili hizo.
Alisema kwa muda mrefu wapo baadhi ya viongozi kutoka upinzani waliokuwa wakilalamika kwamba Tanganyika imevaa koti la Muungano, “Basi katika Katiba Inayopendekezwa koti hilo limepunguzwa.”
Aidha, Dk Shein amesema amekubaliana na kuridhishwa na Katiba Inayopendekezwa ambayo imetoa kipaumbele kwa Zanzibar kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
Alisema mambo yaliyobakia katika Muungano ni muhimu sana ikiwemo ulinzi na mambo ya elimu ya juu ambayo yatasaidia kuwawezesha vijana kupata elimu ya juu kwa kutumia bodi mbili za elimu.
Chanzo:Habari Leo
0 comments:
Post a Comment