Home » » ‘ZANZIBAR HAITARUHUSU MAFUTA, GESI’

‘ZANZIBAR HAITARUHUSU MAFUTA, GESI’

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Maalim Seif Sharif Hamad

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema Zanzibar haiwezi kuruhusu kuchimbwa mafuta na gesi asilia kabla haijawa na sheria na sera juu ya mafuta hayo.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika kiwanja cha Gombani ya Kale kisiwani Pemba, alisema ni lazima kuwe na sheria zinazotamka wazi jinsi Wazanzibari watakavyonufaika na mafuta na gesi hiyo.
Maalim Seif, alisema ni lazima kuwe na chombo cha Wazanzibari ambacho kitashughulikia uchimbaji wa mafuta na usimamizi mzuri utakaohakikisha kila Mzanzibari ananufaika na mafuta na gesi, ikiwemo suala la ajira.
Akizungumzia Katiba inayopendekezwa, alisema ni koti linalozidi kuibana Zanzibar, badala ya kuipa nafuu na kamwe Wazanzibari hawawezi kuikubali.
Alisema Katiba hiyo ina mambo mengi ambayo yanainyang’anya mamlaka yake Zanzibar, na wale wanaopita kusema kuwa Zanzibar imepata kila inachokitaka kwenye Katiba hiyo ni waongo.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema Katiba hiyo imekiuka hata ile misingi mikuu ya mkataba wa Muungano ambayo inatambua Mamlaka ya Zanzibar ndani ya Muungano.
Alisema pamoja na viongozi wa CCM wanaopita na kusema kuwa Katiba hiyo imeyatoa mafuta na gesi asilia sasa kuwa si ya Muungano, jambo hilo ni sawa na kuipaka mafuta Zanzibar, kwa sababu ardhi sasa imefanywa ni jambo la Muungano.
“Sheria za Zanzibar ziko wazi kabisa juu ya ardhi kumilikiwa na Wazanzibari, lakini kwenye Katiba inayopendekezwa suala hilo sasa ni la Muungano, licha ya kuwa ardhi ya Zanzibar ni ndogo sana na haitoshi hata kwa Wazanzibari wenyewe,” alisema Malim Seif.
Aliongeza kuwa si kweli kwamba kuna msururu wa kampuni za kuchimba mafuta na gesi asilia, baada ya kusikia sekta hiyo imetolewa kwenye Muungano.
Katika hatua nyengine, Maalim Seif alisema kwamba matukio yaliyojiri Dodoma juu ya mchakato wa Katiba, yatawafanya Wazanzibari kushikamana na kuitetea Zanzibar, jambo ambalo wanajua litaweza kufanikiwa iwapo chama cha CUF kitakamata Serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jusa Ladhu, aliwapongeza wananchi wa kisiwa cha Pemba kwa kuwa imara miaka yote na kuonesha ukomavu mkubwa na msimamo usioyumba katika kuhakikisha hadhi ya Zanzibar ina baki na wao wamekuwa ngome imara ya kuitetea Zanzibar na maslahi yake.
“Pemba hakuna kituko au kitimbi ambacho hawajafanyiwa Wapemba, lakini hilo kamwe halikuwatoa kwenye mstari na wameweza kuhimili dhoruba hizo na hivi sasa kuna kila dalili chama cha CUF kitashika serikali katika uchaguzi mkuu hapo mwakani.
Alieleza kwamba, uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa upande wa Zanzibar utakuwa ni kati ya wanaotaka Mamlaka kamili na wale madalali wa Zanzibar waliokwenda kuiuza Dodoma.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, ambae pia ni Waziri wa Biashara katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alisema mambo yaliyokuwa yakifanyika Dodoma si mambo ya kufanywa na watu waungwana, hasa kitendo cha baadhi ya wajumbe kuuza nchi yao ya Zanzibar kwa kujali maslahi yao wachache
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa