Home » » KARAFUU YA ZANZIBAR YAZIDI KUPATA UMAARUFU

KARAFUU YA ZANZIBAR YAZIDI KUPATA UMAARUFU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MSHAURI wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar, Sadruddin Govinji, amesema karafuu ya Zanzibar imeendelea kupata umaarufu katika soko la Dunia kutokana na sifa zake za kipekee zenye ubora.
Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa majukumu kwa Kamati ya Fedha, Kilimo na Biashara ya Baraza la Wawakilishi (BLW), Zanzibar katika Tawi la ZSTC lililopo ‘Al-Qusais Industrial Area’ Dubai, Mshauri huyo alisema Wananchi wa Dubai na wengineo wanaotembelea nchi hiyo kibiashara wamekuwa wakivutiwa kununua karafuu ya Zanzibar ukilinganisha na ya kutoka nchi nyingine.
Alisema hatua ya ZSTC kuweka karafuu za vifungashio vya ujazo mdogo (Small packaging), imewavutia wateja wengi kwa vile ni rahisi kwa wananchi kununua katika ujazo wanaouhitaji.
Alibainisha kuwa ujazo huo mdogo wa kilo moja, nusu na robo kilo kutokana na ulivyosanifiwa, umekubalika sana nchini Dubai na unachukua nafasi ya pili kukubalika miongoni mwa viungo vinavyouzwa nchini humo.
Alisema tawi hilo linaendelea na mipango ya kuitangaza zaidi na kuuza karafuu ya Zanzibar, ikiwemo katika maduka makubwa na ya viwanja vya ndege na kushiriki katika maonyesho mbalimbali yanayofanyika nchini humo.
Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji ya Ofisi hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mwendeshaji, Naibu Mkurugenzi Fedha, Ali Suleiman, alisema kuwa ZSTC ilifungua ofisi hiyo mwaka 1993 kwa madhumuni ya kuwa kituo cha Shirika katika kutangaza zao la karafuu ya Zanzibar kwa nchi za Falme za Kiarabu.
Nae Ofisa Mwandamizi wa Ubalozi Mdogo nchini Dubai, Clephas Ruhumbika, alilishauri Shirika la ZSTC kuongeza uzalishaji wa karafuu ili kukidhi mahitaji katika soko la dunia.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa