SERIKALI ya Japan kupitia Shirika lake la Kimataifa la
Maendeleo (JICA) limeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha
miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa diko na soko la kisasa la
samaki linalotarajiwa kujengwa Malindi mjini Zanzibar.
Makamo wa Rais wa
Shirika hilo la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), Yasushi Kanzaki
aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Katika maelezo yake,
Makamo huyo wa Rais wa (JICA) ambaye aliongozana na uongozi wa Wizara ya
Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, alimueleza Dk. Shein kuwa Shirika hilo liko
tayari kuanza ujenzi huo mapema mwakani na hivi sasa limo katika hatua za
mwisho za matayarisho.
Makamo huyo alisema
kuwa mradi wa ujenzi wa soko hilo utakuwa ni wa kisasa na wa kuvutia kutokana
na kukidhi mahitaji yote yanayopaswa kuwepo kwa ajili ya diko na soko la samaki
la kisasa.
Alisema kuwa soko hilo
litakuwa la pekee katika ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo
ujenzi wake unatarajiwa kufanyika ndani ya muda wa miaka miwili kuanzia muda
utakaoanza ujenzi huo.
Aidha, Bwana Yasushi
Kanzaki aliahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi
mengine muhimu ya maendeleo ukiwemo mradi wa kilimo cha mpunga wa umwagiliaji
maji, uvuvi na kuendeleza mradi wa usambazaji maji kupitia Mamlaka ya Maji
Zanzibar (ZAWA).
Katika mazungumzo yake
kiongozi huyo, alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Shirika hilo katika
kuimarisha mradi wa maji utakaokwenda sambamba na teknolojia mpya ya kisasa ili
kurahisisha usambazaji na upatikanaji wa maji safi na salama hapa nchini.
Sambamba na hayo,
Makamu huyo wa Rais wa Shirika la (JICA), alimueleza Dk. Shein matayarisho
yanayoendelezwa na Shirika lake na hatua zilizofikiwa katika kuimarisha mradi
wa kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji kwa mabonde maalum yaliotengwa hapa
Zanzibar.
Nae, Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi na
shukurani kwa Serikali ya Japan kupitia shirika lake la (JICA) na kueleza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake wanathamini sana misaada na
ushirikiano na uhusiano uliopo kati yake na (JICA).
Alisema kuwa Shirika
la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) ni mshirika muhimu wa maendeleo hapa Zanzibar
kwani limeweza kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ya kilimo, maji, afya,
elimu, uvuvi na mengineyo.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kupongeza azma ya ujenzi wa soko hilo ambapo alisema kuwa utasaidia
kuendeleza malengo ya serikali katika kuimarisha sekta ya uvuvi na kusisitiza
kuwa tayari miundombinu ya eneo linalotarajiwa kujengwa soko ikiwemo umeme na
maji lipo katika hatua za mwisho za matayarisho pamoja na kueleza kuwa tayari ruhusa
kutoka UNESCO nayo imeshatolewa.
Dk. Shein alisema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka lengo la kuanzisha programu ya uvuvi
wa bahari kuu ambayo pia, itawasaidia wavuvi kuvua katika kina kirefu cha maji
ili kuongeza kiwango cha samaki wanaovuliwa na kuongeza fursa za ajira, biashara
na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wa kilimo
cha mpunga wa umwagiliaji maji, Dk. Shein alisema kuwa tayari Serikali imo
katika juhudi za kuweka miundombinu kwa kuimarisha eneo la hekta 2,200 katika
mabonde ya mpunga huku akieleza huku
akilipongeza Shirika la JICA kwa kuuunga
mkono mradi huo.
Alisema kuwa lengo la
Serikali katika kuimarisha kilimo hicho ni kupunguza ama kuondosha kabisa
uagiziaji wa mchele kutoka nje ya nchi unaofanyika hivi sasa kwani matumizi ya
mchele hapa nchini ni tani 80 elfu kwa mwaka ambapo kati ya hizo tani 64 elfu
huagizwa na zinazozalishwa nchini ni tani elfu 16 tu.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa Shirika hilo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar
katika kuendeleza mradi wa maji safi na salama, kwa awamu zote huku akieleza
hatua inayofuata ya kuimarisha mradi huo kwa utaalamu zaidi utasaidia upatikanaji
wa huduma hiyo kwa ufanisi zaidi.
Madhumuni makubwa ya
mradi wa ujenzi wa diko na soko la kisasa huko Malindi ni kuwawezesha wavuvi
wanaotumia soko hilo kuuza na kununua samaki wao wakiwa salama kiafya pamoja na
kuwepo mazingira mazuri ya kuweka vyombo vya uvuvi na biashara kwa wavuvu,
wachuuzi, madalali, wauzaji wadodgo wadogo na wanunuzi.
Tsh. Bilioni 14
zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa soko hilo ambalo litakuwa na maeneo sita
ya kuendesha mnada, meza ndogo 141 za wauzaji wadogo wadogo, sehemu 13 za
kuchakatia samaki, linatarajiwa kwa siku litakuwa kuegesha vyombo vya uvuvi wa
kienyeji 392 na wafanyakazi 1,400 watakaoshusha na kupakia samaki ambapo pia,
wafanyabiashara 6,500 watatumia eneo hilo salama.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 comments:
Post a Comment