Home » » CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewasihi viongozi wake kutojali wala kukatishwa tamaa na maneno yanayotolewa na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya Chama

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewasihi viongozi wake kutojali wala kukatishwa tamaa na maneno yanayotolewa na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya Chama

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na Is-haka Omar, Zanzibar.
 
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  kimewasihi viongozi wake kutojali wala kukatishwa tamaa na maneno yanayotolewa na  baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya Chama hicho badala yake wayatumie kama fursa ya kuongeza kasi ya utendaji wa majukumu yao.
 
Nasaha hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,  Nd. Vuai Ali Vuai wakati akizungumza na  Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mjini Kichama wakati kuhitimisha ziara ya  kuimarisha uhai wa Chama iliyofanyika katika Mikoa yote kichama Unguja na Pemba.
 
Amefafanua kuwa kuna kauli na njama zisizofaa zinazotolewa na wapinzani wakiwatuhumu baadhi ya viongozi wa chama kuwa walihusika na njama za kuharibu Uchaguzi Mkuu uliopita jambo ambalo sio la kweli.
 
Alisema kauli hizo zisiwavunje moyo viongozi wa CCM hasa wa Mkoa huo bali wazitumie kama sehemu muhimu ya kujiongeza kiuongozi na kubuni njia mpya za kiutendaji zitakazosaidia Wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Chama hicho.
 
“ Tuendelee kufanya kazi kwa bidii na kwa mujibu wa miongozo ya Katiba na Kanuni za Chama Chetu, wala tusiyape nafasi ya kututawala maneno na kauli za wapinzani kwani wanakesha wakipanga njama za kila aina ili tupoteze muelekeo wa kisiasa lakini kwa uwezo wa Mungu hawatoweza kamwe.”, alifafanua Vuai.
 
Aidha alisema Chama hicho kina uzoefu mkubwa wa kisiasa na kinajivunia maendeleo yaliyopatikana kutokana na viongozi wake walio Mikoani na Wilayani ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiwasimamia kwa uadilifu na weledi viongozi waliopo chini yao.
 
Nd. Vuai aliwambia viongozi kuwa pamoja na kuwepo na changamoto mbali mbali katika Mikoa yao bado wana jukumu la kufanya kazi kwa bidii kwa lengo kuimarisha Chama ndani ya maeneo yao.
 
Aliwataka viongozi na watendaji wa Chama Cha Mapinduzi Kuongeza kasi ya kutafuta  wanachama wapya ambao wametimiza umri kisheria ili waweze kujiunga na CCM kwa lengo la kukipigia kura Chama katika Uchaguzi Mkuu ujao.
 
Hata hivyo alisisitiza suala la kuhamasishwa  kwa viongozi watakaopewa majukumu ya kusimamia Uchaguzi wa Chama wasiwanyime fursa wanachama wenye nia na sifa za uongozi  kugombea nafasi mbali mbali ndani ya CCM.
 
Naibu Katibu Mkuu huyo, aliwapongeza viongozi wa Mkoa huo kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu uliopita na kupatikana viongozi makini wa CCM pamoja na kusimamia ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015/2020 kwa wananchi wote bila ya ubaguzi.
 
Pamoja na hayo aliwataka  Wana CCM na Viongozi wote wa Chama hicho kuendelea na Maandalizi ya kuandaa mazingira mazuri ya kukipatia ushindi katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.   
 
Ziara hiyo imefanyika katika Mikoa yote kichama  ya Zanzibar, kwa lengo kuimarisha chama, kuzungumza na kubadilishana mawazo na viongozi pamoja kuwashukru na kuwapa pole Wana CCM waliofanyiwa fujo, hila na kujeli na wapinzani kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa